UFICHE KAMA MKAKATI WA UPOLE KATIKA MATUMIZI YA LUGHA: MFANO WA MAWAIDHA YA BI. MSAFWARI NA ULUMBI WA BW. MANGULIECHI
Abstract
Fasiri ya maana iliyokusudiwa ni jambo la kimsingi linalopaswa kutathminiwa na
kupewa umuhimu na mtoa kauli katika mawasiliano yoyote. Ijapokuwa mwasilishaji
ujumbe anapaswa kuteua mkakati unaomsaidia kuhawilisha ujumbe katika hali ya
kufasirika vyema, kuelewesha maana na kuondoa utata katika mawasiliano, hali hii
haijitokezi katika mkakati wa ufiche unaowasilisha ujumbe kwa njia isiyo wazi. Lengo la
utafiti lilikuwa kuchunguza ufiche kama mkakati wa upole katika matumizi ya lugha ya
ulumbi wa Bw. Manguliechi na mawaidha ya Bi. Msafwari. Madhumuni yalikuwa;
kupambanua maumbo yanayobainisha mkakati wa ufiche, kubainisha miktadha ya
matumizi ya ufiche na kutathmini sababu za matumizi ya ufiche katika matumizi ya
lugha katika ulumbi wa Bw. Manguliechi na mawaidha ya Bi, Msafwari. Utafiti ulitumia
muundo wa uchanganuzi kifani. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Upole
iliyoasisiwa na Brown na Levinson (1978) wakaieneleza zaidi mwaka 1987. Mihimili
mitatu ilitumiwa; mhimili wa uainisho wa maumbo ya ufiche, mhimili wa hali na
muktadha pamoja na sababu zilizosababisha uteuzi wa mkakati wa ufiche katika
mawasiliano. Utafiti ulihusisha eneo kitaaluma. Taaluma husika katika utafiti huu ilikuwa
ya uchanganuzi wa matini ambapo matini katika utanzu wa mazungumzo
zilichanganuliwa. Ulumbi na mawaidha yaliteuliwa kimakusudi kwa ajili ya dhima yake
katika kuendeleza elimu ya kiasili kwa jamii. Umma lengwa ulikuwa utanzu wa
mazungumzo. Usampulishaji wa makusudi ulifanywa kuteua ulumbi wa Bw.
Manguliechi na mawaidha ya Bi. Msafwari. Data ilikusanywa kupitia mbinu ya
uchanganuzi wa yaliyomo katika rekodi za kanda za maktaba ya Kituo cha Habari cha
West FM, rekodi za mtandao za Mawaidha na Bi. Msafwari, mahojiano ya simu na Bi.
Msafwari pamoja na mahojiano fuatilizi ya kundi teule. Data ilichanganuliwa kwa
kutumia mbinu ya kufasili. Matokeo ya utafiti yamewasilishwa kwa njia ya maelezo ya
aya na majedwali. Matokeo yalibainisha kuwa chuku, maswali ya balagha, mkazo kinzani
na methali ni baadhi ya maumbo ya mkakati wa ufiche yaliyobainishwa ijapokuwa kwa
miundo tofauti katika ulumbi wa Bw. Manguliechi na mawaidha ya Bi. Msafwari.
Ilibainika kuwa, muktadha wa hali miongoni mwa aina nyingine za miktadha ulichangia
pakubwa katika uteuzi wa mkakati wa ufiche. Miktadha ya kiisimu na kitamaduni
ilidhihirisha matumizi ya ufiche kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza elimu ya kiasili.
Sababu tofauti zinazomsababisha mtoa kauli kuutumia ufiche zilidhihirika kufungamana
na muktadha wa matumizi yake. Ufiche ulitumiwa kuhimiza, kushutumu, kuimarisha
madai na kuelekeza uzingativu kwa neno husika. Utafiti huu unahitimisha kuwa,
upambanuzi wa maana kusudiwa katika kauli zenye ufiche ni swala tata. Utafiti huu
unapendekeza kuwa, upambanuzi wa vipengele vya kimuktadha utiliwe maanani na
mpokea ujumbe ili kupunguza utata na kuielekeza fasiri yake kwa maana kusudiwa.
Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuchangia upambanuzi wa mkakati wa ufiche katika
lugha. Aidha, yatachangia elimu ya uchanganuzi matini katika Kiswahili na lugha za
Kiafrika. Kutokana na faida ya matumizi ya ufiche, wawasilishaji ujumbe wanaweza
kutumia njia hii kama mbinu ya kuwasilisha maana kuhusu masuala muhimu ya jamii
kwa njia inayoacha athari kubwa, ilivyo katika ulumbi wa Bw. Manguliechi na mawaidha
ya Bi. Msafwari. Aidha data iliyochunguzwa inaweza kutumiwa baadaye na wanaisimu
katika isimu linganishi kwa tafiti za lugha za kiasili
Collections
- School of Education [67]