Aina ya Nyezo katika Ufundishaji wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili Katika Shule za Sekondari Nchini Kenya
Date
2020-10-24Author
Bakari, Osundwa Kassim
M'raiji, John Kirimi
Luganda, Manasseh
Metadata
Show full item recordAbstract
Madhumuni ya makala haya yalikuwa kubaini aina ya nyenzo katika ufundishaji wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili katika Shule za Sekondari katika Kaunti ya Kakamega nchini Kenya kwa kuangazia madarasa ya mwanzo. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Maendeleo ya Kiutambuzi ya Jean Piaget (1896-1980) iliyoasisiwa mwaka 1954 inayosisitiza umuhimu wa kutangamana na matini husika kwa lengo la kuelewa katika hatua za mwanzo za funzo. Utafiti huu ulitumia muundo wa usoroveya elezi. Idadi lengwa ya utafiti huu ni walimu wa somo la Kiswahili pamoja na wanafunzi wa madarasa ya mwanzo katika shule za sekondari katika Kaunti ndogo ya kati ya Kakamega. Mtafiti alitumia mbinu za usampulishaji za kinasibu na kimakusudi kuteua sampuli ya kutumiwa ambayo ilikuwa theluthi moja ya idadi lengwa. Walimu ishirini na tano (25) ambao ni theluthi moja ya walimu wote wanaofundisha Kiswahili katika madarasa ya mwanzo katika shule za sekondari Kaunti ndogo ya kati ya Kakamega na wanafunzi mia mbili hamsini (250) walishirikishwa na data kukusanywa kwa kutumia miongozo ya uchunzaji, hojaji, mahojiano na uchanganuzi wa nyaraka. Data ziliwasilishwa kwa kutumia maelezo, majedwali, vielelezo na viwango vya kiasilimia. Matokeo ya utafiti huu yalikuwa kwamba, walimu wanatumia aina tatu za nyenzo katika ufundishaji wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili lakini hawatilii mkazo nyenzo zinazotokana na hali na mazingira mbalimbali ya mfumo wa kijamii katika kufundisha Fasihi Simulizi ya Kiswahili licha ya kuwepo. Utafiti huu utakuwa muhimu kwa sababu mbali na kuwapa walimu uelewa mpana wa aina ya nyenzo katika ufundishaji wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili, utasaidia katika kutambua hali na mazingira inayopatikana kama nyenzo katika ufundishaji na hivyo kuimarisha juhudi za wadau katika sekta ya elimu katika kuboresha matumizi yake. Utafiti ulipendekeza serikali kutenga sehemu maalumu katika Kaunti ili kuwapa walimu nafasi ya kutangamana na aina tofauti ya nyenzo zinazotokana na mifumo ya kijamii kwa kufundisha Fasihi Simulizi ya Kiswahili kwa kuimarisha na kuhifadhi mazingira ya kijamii kwa lengo la kutumika kama nyenzo.
URI
https://doi.org/10.37284/eajss.2.2.227https://journals.eanso.org/index.php/eajss/article/view/227
http://ir-library.mmust.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/1979
Collections
- Journal Articles [411]