UCHANGANUZI WA MAKOSA YA KISARUFI KATIKA INSHA ZA WANAFUNZI WA GREDI YA SITA WA MTAALA WA UMILISI WA SHULE ZA MSINGI KATIKA GATUZI DOGO LA BUTULA BUSIA
Abstract
Lugha ya Kiswahili ina dhima muhimu katika jamii kwa hivyo changamoto zinazoikabili kwa
vyovyote vile zinastahili kutatuliwa. Mojawapo ya changamoto hizi ni athari ya lugha ya kwanza
kwa ujifunzaji wake. Hali hii huathiri wanafunzi kwenye viwango vyote vya elimu ikiwemo shule
za msingi na hudhihirika kwa namna mbalimbali ikiwemo katika uandishi wa insha. Ukiukaji wa
sheria za kisarufi za Kiswahili huchangia hali hii. Hivyo basi, Lengo la utafiti huu lilikuwa
kuchunguza makosa ya kisarufi katika insha za wanafunzi wa shule za msingi katika mtaala mpya
wa elimu ya umilisi katika Gatuzi dogo la Butula. Madhumuni yalikuwa; kubainisha makosa ya
kisarufi katika insha za wanafunzi wa gredi ya sita wa Kiswahili wa mtaala wa elimu ya umilisi,
kuchunguza chanzo cha makosa ya kisarufi katika insha za wanafunzi wa gredi ya sita wa
Kiswahili wa mtaala wa elimu ya umilisi na kupendekeza mikakati ya kupunguza makosa ya kisarufi katika insha za wanafunzi. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Makosa
(NUM) ambayo iliasisiwa na Corder (1967), ambaye anasema kuwa kufanya kosa ni njia
mojawapo ya kujifundisha lugha ya pili. Kwa hivyo, mwanafunzi anapofanya kosa, asiadhibiwe
bali chanzo cha kosa kibainishwe. Muundo wa utafiti ulikuwa wa usoroveya elezi. Eneo la utafiti
lilikuwa gatuzi dogo la Butula. Kundi lengwa lilikuwa wanafunzi 1100 wa gredi ya sita pamoja na
walimu 72 wa Kiswahili wa shule 72 za msingi za kutwa. Mbinu za ukusanyaji data zilikuwa:
uchunzaji, hojaji, usaili na uchanganuzi nyaraka. Vifaa vya utafiti vilivyotumiwa vilikuwa hojaji,
orodha ya uchunzaji, mwongozo wa usaili na mwongozo wa uchanganuzi nyaraka. Sampuli za
kimaksudi, kitabakishi na nasibu zilitumika. Usampulishaji kimaksudi ulitumika kuchagua shule
22 za msingi za kutwa na walimu 22 wa kiswahili. Usampulishaji kitabakishi ulitumika kugawa
shule katika makundi huku usampulishaji nasibu ukitumika kuchagua wanafunzi 330 walioshiriki
kwenye utafiti. Data ilichanganuliwa kutumia mbinu ya uchanganuzi wa yaliyomo na uchanganuzi
wa kiidadi. Kipengele cha uchanganuzi kilikuwa matini zenye makosa ya kisarufi. Matokeo ya
utafiti yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo katika aya, majedwali na chati. Matokeo ya utafiti
yalibaini makosa ya kisarufi katika insha za wanafunzi wa mtaala wa umilisi kama ya kifonolojia
(ubadilishaji wa sauti, udondoshaji wa sauti, uchopekaji wa sauti, uyeyushaji). Makosa ya
kimofolojia (kudondoa viambishi katika neno, kuunganisha na kutenganisha maneno visivyofaa).
Makosa ya kisintaksia (upatanisho wa kisarufi katika sentensi). Makosa ya kisemantiki (matumizi
ya msamiati usiofaa na mrundiko wa maneno katika sentensi). Chanzo cha makosa ya kisarufi
yalitambuliwa kama: kutofahamu wakati wa kutumia sauti zingine, mielekeo ya wanafunzi, mbinu
zisizofaa za ufundishaji miongoni mwa mengine. Matokeo yalionyesha kuwa makosa ya kisarufi
yanaweza kutatuliwa kwa njia anuai kama: uhamasishaji wa wazazi kuhusu mfumo wa elimu ya
umilisi, uandishi wa insha mara kwa mara, miongoni mwa mengine. Utafiti unahitimisha kuwa
makosa ya kisarufi katika insha za wanafunzi wa Kiswahili katika mtaala wa elimu ya umilisi
gatuzi dogo la Butula ni mengi na yanajumuisha makosa ya kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia
na kisemantiki. Ingawa makosa mengi yametokana na athari ya lugha ya kwanza mengine
yametokana na vyanzo mbalimbali. Mikakati mwafaka ikitumika kukabili tatizo hili, wanafunzi
wataweza kuepuka makosa mengi. Uhamasishaji wa wazazi kuhusu elimu ya umilisi ni mojayapo
ya mikakati mwafaka ya kurekebisha makosa haya. Kutokana na matokeo ya utafiti huu, makosa
ya kisarufi yalijitokeza katika insha za wanafunzi kisha vyanzo vyake kuchunguzwa,
Mapendekezo yalitolewa ili kupunguza makosa haya kama vile Wizara ya Elimu kufuatilia na
kuchunguza namna mwalimu anafundisha. Utafiti huu utawafaa washikadau wa elimu kama vile
wanafunzi, walimu pamoja na maafisa wa elimu ili kubuni sera zinazofaa kuimarisha ufunzaji wa
Kiswahili.
Collections
- School of Education [74]
